Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Ephraim Balozi Mafuru amesema kuwa mikutano ya kimataifa inayofanyika nchini lengo lake sio tu kukodisha ukumbi bali inawalenga washiriki wa mikutano hiyo kuona vivutio mbalimbali vya utalii, fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kununua bidhaa mbalimbali na kupata huduma ambazo Tanzania inazitoa.
Mkurugenzi Mkuu Mafuru ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihojiwa mubashara na kituo cha Redio cha East Africa kijulikanacho kama “Supa Breakfast” kuhusu mkutano mkubwa wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Mtaji Rasilimali Watu utakaofanyika jijini Dar es Salaam Julai 25 na 26, 2023.
- Advertisement -
Ad image
Mafuru ameshukuru juhudi kubwa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuweza kuvutia mikutano ya kimataifa kufanyikia Tanzania ikiwemo huu wa wakuu wa nchi kujadili kuhusu Rasilimali Watu.
“Tanzania ina nafasi ya kipekee Afrika kama nchi yenye amani, uongozi thabiti, kitovu cha utalii pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo imewadhihirishia mataifa mengine duniani kwamba hii ni sehemu sahihi ya mambo mengi. Mikutano mikubwa kufanyikia Tanzania inaleta faida kubwa katika mnyororo mzima wa uchumi wa nchi hii katika sekta mbalimbali,” alisema Mafuru.
Amefafanua kuwa kumbi za mikutano katika kituo hicho ni za kisasa, mathalan kwa hapa jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere kuna vyumba viwili vyenye hadhi ya VIP ambavyo vina ulinzi wa kutosha, milango ya kuingilia na kutoka kwa ajili ya watu muhimu (VIP) tu na vyumba zaidi ya 20 ambavyo vina hadhi ya kuwaweka viongozi wakubwa.
Aidha ameeleza kuwa, kwa uandaaji wa mikutano barani Afrika, Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 13 miaka minne iliyopita hadi kufika nafasi ya 5 ikiwa ni asilimia 10 ya mikutano yote inayofanyika Afrika, bara lenye jumla ya nchi 54. Hii yote imetokana na matokeo ya uzinduzi wa filamu ya Royal Tour iliyochangia kuitangaza Tanzania duniani kote.
Kwa ridhaa ya Serikali, taasisi hiyo imedhamiria kuwekeza katika ujenzi wa kituo kipya cha mikutano jijini Arusha kitakachojulikana kama “Mount Meru Convention Center” kitakachobeba watu 3,000.
0 maoni:
Chapisha Maoni