Torinto hot media Blog.
Na Jerome Mlaki wa DAR.
Waziri Makamba ameitaka menejimenti ya REA ikakae na kutafakari namna gani wanaweza kufanya mabadiliko katika usimamizi wa kazi za REA na waje na kitu kinaitwa REA 2.0 ambayo inamaanisha REA mpya. Onekaneni. Kuweni na meno. Alisisitiza Waziri Makamba
Pia, amewataka waratibu wa miradi ya REA katika kila mkoa na Wilaya kuweka mfumo wa mawasiliano ya moja kwa moja baina yao na makao Makuu ya Wizara kusimamia utekelezaji.
Naye Naibu Waziri wa Nishati Wakili Stephen Byabato amesema kulikuwa na changamoto mbalimbali kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi ya REA hivyo hatua ya kuwa pamoja na wakandarasi na kuwasimamia kutasaidia katika utekelezaji mzuri wa Miradi ya REA.
Amewataka wakandarasi hao kukamilisha miradi kwa wakati na kuwa jukumu la usimamizi wa utekelezaji wa Mradi huo wa Peri Urban III litakuwa ni jukumu lake la msingi ikiwa ni katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwafikishia wananchi wote umeme.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kwa miaka mingi kuna maeneo ya pembezoni mwa miji ambayo yana maendeleo mazuri, nyumba nzuri zimejengwa na pana wateja wazuri wenye uwezo wa kutumia umeme, lakini kwa sababu mbalimbali, TANESCO imekwenda mpaka kiwango fulani na bado kuna maeneo haijayafikia.
Mramba ameeleza kuwa hii si kwa sababu TANESCO haioni haja ya kupeleka umeme katika maeneo hayo, bali ni kutokana na ukweli kuwa, majukumu ya TANESCO ni mengi na yanaenda kwa hatua.
“Mradi huu, unasaidia kuwafikishia umeme wateja wale ambao kwa kiasi kikubwa wapo tayari kupokea umeme lakini tu miundo mbinu ya umeme haijafika maeneo hayo. Mradi wa Peri Urban ambao umeenda hatua kwa hatua, naamini ni jibu la kuweza kufikisha umeme katika maeneo hayo.” Alisema Mha. Mramba.
Katibu Mkuu Mramba amesema, nia ya uongozi wa Wizara ya Nishati ni kuona kuwa kazi hii inafanyika kwa kasi kubwa kwa sababu miundombinu ipo na kazi ya Wakandarasi ni kufanya muendelezo (extension) kwa ajili ya kuwafikia wateja husika hivyo ni matarajio ya Wizara ya Nishati kuwa, kazi hiyo itafanyika kwa haraka, lakini pia kwa ubora na kwa umakini. Ili wateja hao wapate umeme katika viwango vinavyokubalika.
Katibu Mkuu Mramba amewataka wakandarasi hao kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, kwa ubora na kwa kukidhi matarajio na malengo ya miradi ilipokuwa inaanzishwa.
Mradi wa Peri Urban III ni jibu katika kufikisha umeme katika maeneo ambayo TANESCO imepeleka umeme kwa kiwango fulani lakini kuna maeneo ambayo haijayafikia si kwa sababu TANESCO haitaki kufikisha umeme katika maeneo hayo bali ni kutokana na ukweli kuwa majukumu ya TANESCO ni mengi na yanakwenda kwa hatua
Awali, akizungumza na wakandarasi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mha. Hassan Saidy, aliwataka wakandarasi kutumia hekima na ushirikishwaji wa wananchi husika pamoja na viongozi wao ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima wakati wa utekelezaji wa mradi.
Mha. Saidy, amewataka wakandarasi hao kushusha vifaa katika maeneo husika ya mradi ili kuepuka usumbufu wa kuwa na mvutano na wananchi unaotokana na wakandarsai kushusha vifaa kwenye eneo lisilo la mradi na baadae kutaka kuvihamisha kwenda kwenye eneo la mradi.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wengine waliosaini mikataba ya Peri Urban III na REA, Mrisho Masoud wa Kampuni ya OK Electrical and Electonics Services LTD, amemwakikishia Waziri Makamba kuwa watatekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na pia wametambua kuwa Waziri Makamba hana mzaha katika kazi.
Mradi wa Peri Urban awamu ya tatu utapeleka umeme kwenye maeneo 416 katika mikoa 8 ya Mtwara, Singida, Mbeya, Geita, Tabora , Kagera, Kigoma na Tanga ukihusisha ujenzi wa njia za msongo wa kati wa umeme zenye urefu wa 447km, njia za msongo mdogo wa umeme za urefu wa 1020km, kufunga transformer 417 pamoja na kuunganisha wateja wa awali 22,105 kwa gharama ya shilingi Bilioni 76.9.
0 maoni:
Chapisha Maoni