Katika kutekeleza agizo la Serikali la ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi imekutana na wadau wa ukusanyaji maduhuli ili kujadili jinsi ya kutoa elimu kwa wananchi na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika kikako na wadau hao wa Benki na kampuni za simu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi Dkt. Allan Kijazi amesema kuwa bado wizara haijafikia lengo la ukusanyaji wa mapato toka kwa wananchi kutokana na changamoto ya benki nyingi kuwa mijini na uelewa mdogo kwa wananchi kufanya miamala.
“Kupitia Kodi ya Ardhi tumelenga kusanya bilioni 200 kwakipindi cha mwaka 2021/22 ila tumefanikiwa kukusanya kodi kwa asilimia 60 tu na hii inatokana na changamoto za uelewa mdogo wa kufanya miamala hususani vijijini pamoja na wengi wao kuona usumbufu kufunga safari kwenda mjini kwa lengo la kulipa kodi”Amesema Dkt. Kijazi.
Aidha amewaomba wadau wa kampuni za simu na benki kushirikiana na wizara katika utoaji elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi na jinsi ya kulipa kupitia njia ya benki na simu kwani itaisaidia serikali kuongeza mapato na wao kufaidika kupitia ulipaji huo wa kodi.
“Benki nyingi zinamifumo ya kuelimisha wananchi kwa njia ya kidijitali, sambamba na kampuni za Simu hivyo tunaziomba kutumia njia hizo pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji maduhuli na jinsi ya kufanya miamala ili kukusanya Mapato ya Serikali kwa kiwango stahiki” Ameongeza Dkt Kijazi .
Hatahivyo amesema kuwa kupitia kampuni za simu wataweza kuwafikia wananchi wa vijijini na kuwarahisishia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kulipa kodi hiyo kwenye benki.
Dkt Kijazi amesema baada ya kikao watakuwa wamekubaliana jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja kutaisaidia Wizara ya Ardhi kukusanya kodi ipasavyo kwani idadi ya wananchi wanaolipa kodi bado hairidhishi.
0 maoni:
Chapisha Maoni