NA JEROME MLAKI.... DAR
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimeiomba Serikali kufanya mabadiliko katika sheria ya tozo za miamala ya kibenki kwani zinawaathiri wanachama wao.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa Shani Kibwasali wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Shughuli za chama kwa kipindi cha January hadi Juni 2022 ambapo amesema kuwa katika tozo hiyo mtumishi wa umma hutozwa zaidi ya mara mbili katika pato moja kwa mwezi.
Aidha amesema watumishi wa umma kila mwezi wanalipa kodi kwa kukatwa katika mishahara yao hivyo kupitia tozo hiyo ni kuzidi kumbebesha mzigo na kumkandamiza mfanyakazi ukizingatia mishahara wanayopata haikidhi mahitaji yao ya kila siku na familia zao.
“Suala hili la tozo nalo tunalishughulikia kwa kushirikiana na Vyama vingine vya wafanyakazi kupitia TUCTA ambapo serikali ilipokea maoni na mapendekezo ya vyama na imeahidi kulishughulikia hivyo nawaomba wanachama wetu tuendelee kuwa watulivu tukisubiri utekelezaji wake kwani tunaamini serikali yetu ni sikivu na suala jili litapatiwa ufumbuzi” Amesema Shani.
Hata hivyo amesema kufikia mwezi Juni 2022 walikuwa na kesi 140 ambapo mawakili wa chama wanasimamia kesi 100 na kesi zilizoisha ni 39 na chama kimeshinda kesi 35 na kesi nyingine bado zinaendelea mahakamani.
Katika kushughulikia haki na stahiki za wanachama TALGWU ambazo zipo kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma na kanuni zake imeishukuru serikali kutekeleza upandaji vyeo na mishahara, malipo ya malimbikizo ya mishahara pamoja na utawala bora.
“Pamoja na mafanikio hayo niseme ukweli usiofichika kwamba wanachama wetu ambao ni wahanga wakubwa katika suala la nyongeza za mishahara bado wanamanunguniko na TALGWU kama msemaji wao hatujaridhika kabisa kwa jinsi nyongeza ya mishahara ilivyofanyika” Amesema Shani.
Hata hivyo amewatoa hofu wanachama wa TALGWU kuwa suala hilo linashughulikiwa na chama kwa kushirikiana na Shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi nchini (TUCTA ).
0 maoni:
Chapisha Maoni