Jumanne, 14 Februari 2017
TAARIFA KWA UMMA
1.0. UTANGULIZI
Ndugu Wanahabari na Watanzania wote, Kheri ya mwaka mpya 2017!
Baada ya mapumziko ya sikukuu za Krisimasi pamoja na mwaka mpya, tumewaita leo
hapa, lengo kuu likiwa ni kuwasiliana na umma kupitia vyombo vya habari kuhusu
masuala kadhaa yanayohusu mchakato wa katiba mpya pamoja na maendeleo ya
Tanzania katika ujumla wake. Tumeendelea kufuatilia maendeleo ya mchakato wa
katiba kwa umakini mkubwa, usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanapata
taarifa muhimu na sahihi kuhusu mchakato wa katiba mpya. Katika kufuatilia kwetu
huku, tumebaini pia zipo changamoto zingine za kiutendaji kwa baadhi ya viongozi
waandamizi wa serikali. Aidha, tumeshangazwa sana na kitendo cha Jeshi la Polisi
kuanza kutekeleza agizo la kung’oa matairi kwenye vyombo vya moto vinavyokamatwa
vimepita kwenye barabara ya mabasi ya mwendo kasi. Mbaya, zaidi, agizo hilo lilitolewa
na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, na Jeshi la Polisi kuanza kulifanyia kazi
bila kujali kuwa lipo kinyume na katiba na sheria na kwamba linaweza kusababisha
usumbufu mkubwa kuliko tatizo lenyewe.
Itakumbukwa pia kuwa vitendo vingine kadhaa vimeendelea kufifisha utawala wa sheria
nchini. Kwanza, kamata kamata ya raia na viongozi wanaoonekana kuwa na mwelekeo
wa kukosoa serikali au watawala binafsi. Ingawa JUKATA hatujawahi kutetea
wanaokashifu au kutukana viongozi, uvumilivu na staha kwa wakosoaji wa kawaida
unahitajika sana. Pili, kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali kutaja
majina ya watu na kuwahusisha waziwazi na uhalifu kabla vyombo husika
havijakamilisha uchunguzi ni kinyume cha misingi ya utawala bora na ibara ya 13 (6)
(d) ya Katiba ya Tanzania. Aidha vitendo vya polisi kuadhibu madereva kwa baadhi ya
makosa ya usalama barabarani ambayo hayajatendwa kunazidi kuwatia unyonge
watanzania kiasi cha kujiona kama watumwa ndani ya nchi yao wenyewe kinyume na
uhuru unaoelezwa katika ibara ya 15 (1). Aidha, marufuku kwa mikutano ya kisiasa
inayoendelea nchini siyo tu inabana haki na uhuru wa kujumuika, kutoa maoni na
kueleza fikra zake kwa mujibu wa ibara ya 18 na 20 (1) za Katiba ya Tanzania bali pia
imeua hamasa na ari ya wananchi iliyokuwepo wakati wa uongozi wa awamu ya nne.
Kwa vitendo kama hivi na vingine vingi, hoja ya kuwa na katiba itakayowadhibiti
viongozi wenye kudhani neno lao ndio kauli ya mwisho ama sheria ya nchi inapata
msukumo mkubwa.
2.0. MKANGANYIKO WA KAULI ZA SERIKALI KUHUSU MCHAKATO WA
KATIBA MPYA
Ndugu wanahabari na Watanzania wote,
JUKATA tumeendelea kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakiomba ufafanuzi
wa kauli kinzani juu ya mchakato wa katiba mpya kutoka kwa viongozi wa serikali.
Wananchi wanahoji ipi kauli ya serikali kuhusu mwelekeo wa katiba mpya?. Kwa nyakati
tofauti, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa kauli za kuvunja moyo ama kuleta
faraja juu ya mwelekeo wa katiba mpya. Hivyo, wananchi wanahitaji ufafanuzi na
msimamo wa serikali ya awamu ya tano juu ya mchakato wa katiba mpya. Kwa mfano,
tarehe 23 Juni 2016, Rais alipokuwa akipokea taarifa ya uchaguzi mkuu wa Oktoba
2015 kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) alipongeza jitihada zilizofanywa na
serikali ya awamu ya nne kwenye mchakato wa katiba mpya. Kwa maneno yake,
aliahidi kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya katika kipindi chake cha uongozi.
Lakini pia, kwa mshangao mkubwa na kinyume na maneno yake mwenyewe, tarehe 4
3
Novemba 2016, Mhe. Rais John Pombe Magufuli alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari Ikulu, Dar es Salaam, alisema katiba mpya sio kipaumbele cha serikali yake na
kwamba kwenye kampeni zake hakusema chochote kuhusu katiba mpya.
Kwa kauli hii, na ile ya awali wananchi wengi wamebaki njia panda. Watanzania
wanapenda kuelewa nini msimamo wa serikiali ya awamu ya tano kuhusu mchakato wa
katiba mpya. Ifahamike pia, baadhi ya watanzania ambao walikuwa mstari wa mbele
kudai katiba mpya ya wananchi, kwa nyakati mbalimbali wameendelea kupata uteuzi
ama wa kushika nyadhifa ndani ya Chama Tawala au Serikalini. Wananchi wanahoji je
uteuzi wa namna hii unaashiria nini kuhusu mchakato wa katiba Mpya? JUKATA
tunapenda kumsihi Mhe. Rais ajizuie kutoa kauli ambazo zinawayumbisha na
kuwachanganya wananchi anaowaongoza. Atoe kauli moja kuhusu katiba mpya ambayo
itafuatwa na vyombo vya serikali kama ile ya kung’oa matairi kwenye vyombo vya moto
ilivyoanza kutekelezwa na Jeshi la Polisi.
3.0. KUKOSEKANA KWA TAARIFA RASMI YA SERIKALI KUHUSU
HATMA YA MCHAKATO WA KATIBA
Ndugu wanahabari, achilia mbali uwepo wa kauli kadhaa kuhusu mchakato wa katiba
kutoka kwa viongozi wa serikali, sasa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu serikali ya awamu
ya tano iingie madarakani na hakuna taarifa rasmi ya serikali kuhusu mchakato wa
katiba. Kwa kipindi chote hiki, serikali haijaweza kuweka bayana dira na mwelekeo wa
mchakato wa katiba mpya. Yalikuwa ni mategemeo ya watanzania wengi kwamba
serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Magufuli ingeweza kutoa mwelekeo rasmi
wa mchakato wa katiba katika kipindi cha mwaka mmoja. Lakini serikali imeendelea
kukaa kimya bila kutoa kutoa taarifa rasmi ya serikali. Kukosekana kwa taarifa rasmi
kumeendelea kusababisha wananchi kukata tamaa ya kupata katiba mpya ambayo
ingeweza kutatua changamoto zao kwa kiwango kikubwa. Kama serikali ilivyo na
mipango mingi, ni muda muafaka serikali ikaleta mpango mkakati wa kumalizia
mchakato wa katiba ili wananchi wajiandae vema kushiriki kwenye hatua zitakazofuata
wakiwa na taarifa za kutosha.
4.0. HOJA YA MAREKEBISHO YA SHERIA ZINAZOSIMAMIA
MCHAKATO HAIEPUKIKI
Kama tulivyosema siku za nyuma na kwenye kitabu cha ‘Mwelekeo wa Katiba Mpya
Tanzania’ ipo haja ya kurekebisha sheria zinazosimamia mchakato wa katiba. Tangu
kuanza kwake, mchakato huu wa Katiba umeongozwa na sheria mbili kwa vipindi
4
tofauti. Awali, mchakato ulikuwa ukiongozwa na sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 8 ya
mwaka 2011 (pamoja na marekebisho yake) na baada ya kupitishwa kwa Katiba
Inayopendekezwa, Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013 ikaanza kutumika pia. Hata
hivyo, kwa sasa sheria hizi haziwezi kutumika tena kuongoza mchakato bila kufanyiwa
marekebisho kwa sababu za msingi kuu mbili ambazo ni kupitwa na wakati pamoja na
utata wa sheria hizo hasa sheria ya Kura ya Maoni. Kwa ukweli huu, serikali kupitia
Wizara husika kabla ya bunge la bajeti ipeleke muswada wa kurekebisha sheria hizi ili
kuzipa uhai na ziendelee kuongoza mchakato. Mabadiliko ya sheria hizi hayakwepeki
hata kidogo. Serikali pamoja na bunge ni lazima watekeleze jambo hili haraka
iwezekanavyo.
5.0. MUDA WA KATIBA MPYA NI SASA !
Ndugu wanahabari, tunatambua kuwa mchakato wa katiba mpya ulijisitisha wenyewe ili
kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Kwa uzoefu wetu kutokana na michakato ya
ujenzi wa katiba ndani na nje ya Tanzania, muda muafaka wa kukamilisha mchakato
huu muhimu ni sasa yaani 2017 hadi 2018. Kipindi hiki kisipotumika kukamilisha
mchakato wa katiba, ipo hatari katiba mpya kupatikana baada ya 2020. Hii ni kwa
sababu mwaka 2019 ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Na baada ya uchaguzi
wa serikali za mitaa, joto la uchaguzi mkuu wa 2020 litakuwa juu. Kwa mantiki hiyo,
itakuwa ni hatari kuendelea na mchakato wa katiba katika mazingira ambayo wananchi
watakuwa kwenye maandalizi ya uchaguzi. Mchakato utaingia kwenye mkwamo kama
ule wa mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu. Tunaitaka serikali ya awamu ya tano
ivunje ukimya, iueleze umma wa watanzania mwelekeo wa kupata katiba mpya ni upi,
na lini mchakato utarejea tena. Ni vyema kabla ya kumalizika kwa robo ya kwanza ya
mwaka 2017 serikali ikaweka bayana jambo hili. Katiba mpya ni sasa. Mwaka 2017
unaweza kutumika kurekebisha kasoro kadhaa za kimaudhui katika Katiba
Inayopendekezwa na mwaka 2018 kura ya maoni ikafanyika kupitisha katiba mpya.
Muda ni huu, katiba ni sasa.
6.0. MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU WA KITAIFA WA KATIBA
Ndugu wanahabari,
Kama tulivyosema mwaka jana wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mwelekeo wa
Katiba Mpya Tanzania, njia mojawapo inayoweza kutumika kukamilisha mchakato wa
katiba kwa hali ilivyo sasa ni Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba. Hivyo basi, JUKATA
linapenda kuwajulisha watanzania kuwa, linaratibu maandalizi ya Mkutano Mkuu wa
Kitaifa wa Katiba utakaofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 3 mwezi Machi, 2017 kwenye
5
Hoteli ya Landmark Jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo, wadau watakaopata fursa
ya kushiriki ni serikali, asasi za kiraia, taasisi za kidini, wabunge, vyama vya siasa na
makundi mbalimbali ya kijamii ambao watajadili kwa kina Mchakato wa Katiba
Tanzania: tulipotoka, tulipo, uzoefu kutoka nchi zingine pamoja na tuendako kwenye
mchakato wa kupata katiba mpya. Wasomi wabobevu wa masuala ya michakato ya
kidemokrasia kutoka ndani na nje ya nchi watafanya uchambuzi wa kina tangu kuanza
kwa mchakato wa katiba na kushauri mwelekeo mpya kutoka hapa tulipo. Hii itasaidia
kubaini changamoto tulizopitia na kuzifanyia kazi ili tufikie mwisho wa mchakato wa
katiba mpya. Ni rai yetu kwamba vyombo vya habari viwajulishe wananchi juu ya
mkutano huu muhimu ili waweze kufuatilia taarifa za mkutano huu kwa kushiriki au
kupitia vyombo vya habari muda utakapofika.
7.0. UZINDUZI WA FILAMU KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA
TANZANIA
JUKATA inapenda kuufahamisha umma wa watanzania kuwa, baada ya JUKATA
kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya, hivi karibuni itazindua
filamu fupi ya dakika ishirini yenye lengo la kuonyesha matukio muhimu tangu
mchakato wa katiba ulipoanza. Katika filamu hiyo, JUKATA imeweza kuwahoji watalaam
mbalimbali walioshiriki kwenye mchakato wa katiba katika hatua mbalimbali. Pia,
JUKATA imeweza kupata maoni kutoka kwa wananchi wakielezea ushiriki wao kwenye
mchakato katika hatua zote. Aidha, katika filamu hiyo, wananchi kwa maoni yao
wenyewe wamebainisha namna bora ya kukamilisha mchakato wa katiba ili kupata
katiba mpya. JUKATA inatoa wito kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari
nchini kutumia filamu hii kuendelea kuhabarisha umma juu ya haja ya wananchi
kuendelea kushiriki kwenye mchakato wa katiba mpya bila kujali changamoto
zinazojitokeza.
8.0. SERIKALI ITENGE BAJETI 2017/2018
Wadau wote, wanapaswa kurudi kwenye hamasa iliyokuwepo wakati wa Mchakato wa
kuandika katiba mpya awamu ya kwanza mwaka 2011-2014. Wakati na baada uchaguzi
mkuu wa 2015, hamasa hii imeendelea kushuka. Ni muhimu kwa wadau wote kutumia
muda huu kuanza kumalizia awamu ya pili ya mchakato wa kuandika katiba mpya kabla
hamasa hii muhimu ya wananchi wa Tanzania haijatoweka kabisa. Wadau wote
watambue kuwa, zaidi ya bilioni 100 zilitumika kwenye mchakato wa katiba hasa katika
hatua ya uundaji na uendeshaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK) na uundaji na
uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba (BMK). Fedha hizi zilitokana na kodi za
6
watanzania masikini. Hivyo, kuuacha mchakato wa katiba kama ulivyo sasa ni matumizi
mabaya ya fedha za umma na ni sawa na wizi au utapeli wa kawaida ambao serikali
imewafanyia wananchi wake. Kwa upande mwingine, Serikali kama mdau muhimu
kwenye mchakato wa katiba isiogope gharama ya kukamilisha mchakato wa katiba.
Hatua zilizobaki zinahitaji kwa kiwango kikubwa utashi wa kisiasa kuliko rasilimali fedha.
Ni wito wetu kwa serikali kwamba, katika bajeti ya fedha 2017/2018 itengwe fedha kwa
ajili ya kukamilisha mchakato huu.
9.0. HITIMISHO
JUKATA tunaamini kiongozi bora ni yule atakayekidhi matakwa ya Katiba ya wananchi.
Aidha, JUKATA tunaamini pia kuwa Katiba iliyopo ndiyo muongozo mkuu wa utawala wa
Nchi na haipaswi kusiginwa kwa namna yoyote ile. Kwa vile wananchi bado wana
hamasa ya kupata katiba mpya, ni muhimu kwa viongozi kuhakikisha katiba mpya
inapatikana kwa vile pia Katiba ndio waraka unaowawezesha wananchi kujitambua
kama taifa. Pia, katiba ni waraka wa kiutawala unaoeleza bayana mgawanyo na
majukumu ya vyombo mbalimbali vya dola katika nchi, hivyo katiba ndio waraka mama
wa kisheria na kisiasa unaoongoza shughuli zote za nchi na ni chimbuko la sheria zote
katika nchi. Bila katiba shughuli za serikali na za wananchi haziwezi kufanyika kwa
ufanisi. Ni wito wetu kwa serikali kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya ifikapo mwaka
2018 kwani baada ya hapo siasa za kuelekea ikulu na majimboni zitafanya uwezekano
wa Katiba Kuandikika kuwa mdogo. Katiba mpya ni sasa !
Imetolewa na JUKATA na kusainiwa na;
Deus M.Kibamba
Mwenyekiti wa Bodi
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
0 maoni:
Chapisha Maoni