Torintohot media Blog
Na John Bera - Manyara
Timu ya Maafisa Wandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Zambia vinavyohusika na uzuiaji ujangili wamefika nchini kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika mapambano dhidi ujangili.
Timu hiyo iko nchini kwa siku tano kuanzia Oktoba 29 hadi 4 Novemba 2023.
Akizungumza mara baada ya kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara, Kamishna wa uzuiaji ujangili nchini Zambia, Brigedia Jenerali, Herman Kamwita ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Zambia alisema wamekuja kuona namna Tanzania ilivyofanikiwa kuendesha operesheni za kupambana na ujangili na utekelezaji wa Mkakati wa kupambana na ujangili.
Alisema Kamisheni ya kudumu ya Tanzania na Zambia ya Ulinzi na Usalama ilipendekeza Mamlaka ya nchi hizo mbili kuwa na utaratibu wa kubadilisha uzoefu katika kulinda rasilimali za wanyamapori na misitu.
Alisema wameweza kupitishwa katika mbinu mbalimbali ambazo Tanzania inatumia katika kupambana na ujangili na kuwa wamepanga kwenda kuzitumia wakirudi nchini kwao.
Aliongeza kuwa, "Pia tumepata fursa ya kwenda Hifadhi ya Ziwa Manyara na tumeona wanyama mbalimbali na hii imedhihirisha namna wenzetu walivyopiga hatua kwenye uhifadhi na niwahakikishie kuwa tutakwenda kutumia mbinu hizi ili kuimarisha sekta ya utalii nchini kwetu.’’
Awali, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa Bw. Kiza Yusuph Baraga alisema wamepokea ugeni kutoka Zambia na kuwa kupitia ziara hiyo pande hizo mbili zimebadilishana uzoefu.
"Pia imekuwa ni nia ya nchi yetu kuendelea kutangaza utalii hasa kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza Utalii kupitia filamu ya The Royal Tour. "
Alisema ugeni huo pia umepata fursa ya kujionea vivutio vya utalii baada ya kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara na kushuhudia shughuli mbalimbali za utalii ambazo zinafanywa kwa teknolojia ya hali ya juu.
"Wamefurahi sana na wametuahidi kuwa sehemu ya kutangaza utalii wetu nchini Zambia. Nitoe wito kwa watalii mbalimbali husani wa ndani ya nchi na nje ya nchi kuja kutembelea vivutio vyenye wanyama wengi."
Naye Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrida Lyimo alishukuru wizara kupeleka ugeni huo katika Ikolojia ya Tarangire Manyara na kuwa wameweza kubadilishana mambo mengi.
Kwa upande wake Wakili Mwandamizi Ofisi ya Mashtaka Makao Makuu ambaye pia ni Mratibu wa upelelezi, uendeshaji wa kesi za makosa ya rushwa, udanganyifu na utakatishaji fedha sehemu ya makosa ya mazingira na maliasili wa Kikosi cha Taifa ya Kupambana na Ujangili Theophil Daniel Mutakyawa alisema kupokea ugeni huo na kubadilisha uzoefu ni mwanzo wa kushirikiana katika kupambana na ujangili kwa kubadilishana taarifa.
Alisema makosa ya ujangili ni makosa yanayovuka mipaka yanayohitaji nguvu ya pamoja ya nje ya nchi, kikanda katika kupambana uhalifu huo mkubwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni