WAZIRI MCHENGERWA ATEMBELEA SOKO LA KARIAKOO NA KUPONGEZA UJENZI.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akikagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa Mradi wa soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

NA Jerome Mlaki wa Dar 

Waziri Mchangerwa ameeleza kuwa atamkabidhi pia Mkuu wa Mkoa ripoti yake ambapo amesisitiza wahusika wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani ili kuhakikisha vitendo hivyo vya uchomaji wa majengo na masoko vinadhibitiwa.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila kuhakikisha wote waliohusika na kuungua kwa maduka Kariakoo jijini Dar es Salaam wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Agizo hilo amelitoa leo Novemba 15, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko la ambapo amesema kwamba wahusika wote wanafahamika, hivyo ni lazima wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo kwani kuchoma majengo na masoko ni kosa kubwa.

"Matukio ya moto kuungua kwa masoko yamekuwa yakijitokeza sana, hivyo nimpongeze Mkuu wa Mkoa kwa hatua alizochukua kwa kuunda tume ya uchunguzi na kubaini chanzo cha moto na waliohusika. Pamoja na hatua hizo nimwelekeze kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kwani wanajulikana," amesema Waziri Mchengerwa.


Amebainisha kuwa amekwishatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa wote nchini kuhakikisha wanadhibiti vutendo vya uchomaji wa masoko.

Kuhusu mradi wa ujenzi na ukarabati wa Soko la Kariakoo, waziri Mchengerwa amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kwamba umefikia asilimia 85 ambapo amemtaka mkandarasi kuhakikisha hadi kufikia Februari 2024 unakabidhiwa.

"Nimefanya ukaguzi, nimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi, hivyo ninaimani hadi kufikia Februari mwakani mradi utakuwa umekamilika na Rais ataukabidhi mwenyewe," amesema Waziri Mchengerwa.

Hata hivyo amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anaendelea kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa katika makubaliano ya ujenzi huo ambapo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa soko hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Hawa Ghasia amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha ujenzi wa siko jipya na ukarabati wa soko la awali ambalo liliungua.

"Awali kulikuwa kisoko kidogo, lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa sana. Tutahakikisha wale waliokuwemo wakati soko linaungua ndio wanaopewa kipaumbele siko litakapokamilika, wafanyabiashara wengi watapata nafasi hapa," amesema Ghasia

Waziri Mchangerwa ameeleza kuwa atamkabidhi pia Mkuu wa Mkoa ripoti yake ambapo amesisitiza wahusika wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani ili kuhakikisha vitendo hivyo vya uchomaji wa majengo na masoko vinadhibitiwa.