Waziri Mchengerwa amesema kuwa mradi huo unalenga maeneo mawaili ikiwemo Daraja la juu ambapo amesema lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anamaliza kero ya foleni na mafuriko katika eneo hilo.




NA Jerome Mlaki wa Dar es Salaam.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akizungumza na wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amemwagiza Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanaoathiriwa na mradi wa uendelezwaji wa Bonde la Mto Msimbaji wanaanza kulipwa fidia mara moja.

Kauli hiyo Waziri Mchengerwa ameitoa leo Novemba 15, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo alipokuwa akitoa tamko la kutaka mradi wa uendelezwaji wa bonde hilo uanze mara moja.

"Rais Samia anataka wananchi waishi kwa upendo na amani, hali ya mafuriko inatufanya kama Serikali tufikiri, hivyo tunapaswa kujenga hapa daraja la kisasa litakalodumu kwa miaka 100. Hili linakwenda sambamba na uendelezwaji wa Bonde hili," amesema Waziri Mchengerwa na kuongeza,

"Hivyo nikutake Katibu Mkuu uendelezwaji wa bonde hili la Msibazi uanze mara moja, na uende sambamba na ulipaji wa fidia kwa wananchi, wapo watu asilimia 92 waliopo tayari kulipwa fidia, hawa wapatiwe fedha zao mara moja".

Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa kiutaratubu wananchi waliojenga katika maeneo hatarishi hawastahili kulipwa fidia, hata hivyo amesema kwa upendo wa Rais Dkt. Samia ameamua kuwa hata hao watalipwa fidia ya shilingi milioni 4 ambapo jumla ya wananchi watakaolipwa fidia ni 2400.