Na mwandishi wetu.
Dar es Salaam:
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuwa serikali inapashwa kugharamia jukumu la kuwaunganishia umeme wananchi.
Waziri Kivuli wa Nishati wa Chama hicho Is-haka Mchinjita ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchambuzi wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
“Gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi nchi nzima zinapaswa kuwa jukumu la serikali,” Alisema Mchinjita.
Mchinjita amebainisha kwamba katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 Serikali ilipunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wa vijijini kufikia shilingi 27,000.
Kwamba hatua hii ilipokelewa kwa furaha na wananchi walijitokeza kwa wingi ili kupata huduma hii muhimu.
Ameeleza katika mwaka wa bajeti 2021/2022 Serikali ilizirejesha gharama za awali za kuunganisha umeme kwa kile kilichoelezwa kuwa ni gharama halisi ya kuunganisha umeme.
“Hatua hii iliyoleta maumivu kwa wananchi ni matokeo ya Serikali kukimbia wajibu wake wa kutoa huduma muhimu kwa umma,” ameongeza Mchinjita na kueleza,
“Hatua ya Serikali kuunda kamati ya kufanya tathmini ya maeneo yenye sifa za vijijini kwa maeneo ya mijini ili kufanya gharama ya umeme kushuka ni kupoteza rasilimali bure,”.
Hivyo ameitaka Serikali itekeleze wajibu wake huo.
Kwamba hivi sasa kuna mkanganyiko mkubwa ambapo baadhi ya maeneo kama vile Skonge mkoani Tabora kata moja inagawanywa baadhi ya mitaa kuitwa mjini na mingine vijijini.
Ameitaka Serikali ijifunze kwa matokeo ya ongezeko la watu walioomba kuunganishiwa umeme bei ilipokuwa shilingi 27,000 na upungufu wa maombi baada ya bei kupandisha.
Waziri Kivuli huyo amesema maamuzi haya ya Serikali yana akisi kuwa, Serikali inapopata shida ya kiuchumi inaona njia ni kumkandamiza mwananchi.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme nchini amesema katika zama tulizonazo hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika huchochea ukuaji wa uchumi (Uzalishaji viwandani na mashambani) na utoaji wa huduma zingine kama vile elimu, mawasiliano, usafiri na uchukuzi, matibabu na huduma za utawala.
“Kwa hiyo, umeme una nafasi na mchango mkubwa sana katika maisha yetu kama jamii na nchi kwa ujumla wake,” amesema Mchinjita.
Amesema pamoja na umuhimu huu tunaona huduma ya umeme nchini bado sio ya uhakika kumekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Kwamba kwa hali hii ni wazi kuwa kutosimamiwa vyema huduma ya upatikanaji wa umeme unarudisha nyuma uwekezaji mkubwa kwenye viwanda, kuzoretesha mifumo mingine ya huduma kama vile matibabu, uchukuzi na mawasiliano na masuala ya utawala.
“Mwenendo wa uwezo wetu wa kuzalisha umeme kwa mujibu wa taarifa za wizara kutoka kwenye hotuba ni kuwa, ongezeko la uzalishaji wa umeme nchini kwa mwaka 2021/22 ni megawati 124.92 ni sawa na asilimia 7.94 kwa kulinganisha na uzalishaji wa mwaka uliopita.
Alisema jumla MW 1608.46 wakati uzalishaji wa sasa ni 1,733.38. Wakati, mahitaji ya juu ya umeme katika mfumo wa Gridi ya Taifa yameongezeka na kufikia MW 1,335.01 ikilinganishwa na MW1,201.02 zilizokuwa zimefikiwa mwaka 2020/21, sawa na ongezeko la asilimia 11.16,” Aliongeza Bw Mchinjita.
Aidha, aliongeza kuwa ongezeko la watumiaji kutokana na usambazaji wa umeme vijijini linakuwa kwa asilimia 13.54.
Hivyo ni dhahiri kuwa kasi ya uzalishaji na usambazaji haulingani, jambo linalopelekea kuwa na upungufu wa uwezo wa kuhudumia wananchi, hivyo changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara hutokea.
0 maoni:
Chapisha Maoni