Torinto hot media Blog
Na Jerome Mlaki wa DAR
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Saidi Yakubu amesema Tanzania inakwenda kunufaika kiuchumi na kiutamaduni kwenye msimu ya utamaduni wa Afrika ya kusini unaoanza leo kwa muda wa wiki moja nchini Tanzania.
Yakubu ameyasema haya leo, Novemba 18, 2022 akiwa na Naibu Waziri wa Utamaduni wa Afrika ya Kusini, Mhe. Mcawe Mafu kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari, jijini Dar es Salaam ambapo amefafanua kuwa katika wiki hii kutakuwa na maonesho ya muziki, mavazi, ngoma na kazi za sanaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Zanzibar.
Amezitaja baadhi ya faida ambazo Tanzania itanufaika nazo kuwa kupitia onesho la saana za ufundi mbalimbali, wasanii watapata ajira za muda.
Pia, kupitia maonesho ya kazi za sanaa, utamaduni na ubunifu, wasanii watapata fursa ya kuonesha na kuuza kazi zao za mikono;
Aidha, ameongeza kwamba kupitia msimu huu nchi hizo zinakwenda kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa ushirikiano katika Sekta ya Utamaduni uliosainiwa mwaka 2011.
Faida nyingine ni Wasanii kubadilishana uwezo katika kufanya biashara ya kazi za sanaa na ubunifu kupitia Semina kwa wasanii itakayofanyika Novemba 23, 2022; na kuimarisha mbinu na njia ya uhifadhi na uendelezaji wa historia ya ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika.
Amesema msimu huu unakwenda kufunguliwa rasmi jioni ya leo na Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa
0 maoni:
Chapisha Maoni