Lakini wachezaji wanne tegemeo hawatakuwepo kwenye msafara huo ambao ni beki Juma Abdul, kiungo Thabani Kamusoko, Donald Ngoma na Mrundi, Amissi Tambwe.
Abdul hatakuwemo kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, wakati Kamusoko, Ngoma na Tambwe wote ni majeruhi wa muda mrefu.
Yanga inaendelea na mazoezi asubuhi ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kabla ya safari ya kesho kwenda kupambana na timu inayofundishwa na kocha wao wa zamani, Mholanzi, Hans van der Pluijm.
Yanga inakwenda kwenye mchezo huo, ikitoka kutoa sare na wapinzani wa jadi, Simba kwa kufungana 1-1 Jumamosi iliyopita Uwanja wa Uhuru. Sare hiyo imefanya timu hizo ziendelee kufungana kwa pointi 16 kileleni mwa Ligi Kuu.
Ligi Kuu itaendelea Ijumaa, Maji Maji FC wakiikaribisha Stand United Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, wakati Jumamosi Singida watakuwa wenyeji wa Yanga Uwanja wa Namfua, Singida na Ndanda FC wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Mechi nyingine za Jumamosi, Kagera Sugar wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Njombe Mji FC wataikaribisha Mbao FC Uwanja wa Saba Saba na Azam FC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Jumapili kutakuwa na mechi mbili ambapo Mbeya City watakipiga na Simba, Lipuli FC nao wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
0 maoni:
Chapisha Maoni