MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
TAARIFA YA UZINDUZI WA MAABARA HAMISHIKA (MIN LAB KITS)
Na. Joseph Lieme, Torinto Hot Blog.
TFDA imefanya uzinduzi wa Maabara Hamishika (Minilab Kits) ulifanywa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy A. Mwalimu (Mb.) tarehe 01 Novemba, 2017 katika ukumbi wa TFDA, uliohudhuriwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa TFDA (MAB), Mwakilishi wa Shirika la Afya duniani (WHO), Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Menejimenti na Wafanyakazi wa TFDA pamoja na wanahabari.
TFDA ina jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii dhidi ya madhara yanayoweza kutokana na matumizi ya bidhaa duni na bandia.
Maamuzi juu ya ubora na usalama wa bidhaa mbalimbali zinazodhibitiwa na TFDA hufanywa kwa kuzingatia tathmini za kisayansi pamoja na matokeo ya uchunguzi wa kimaabara. Hivyo, maabara ya TFDA ni kiungo muhimu cha kuwezesha kufanyika kwa maamuzi sahihi katika kulinda afya ya jamii. Kutokana na umuhimu huo, TFDA imekuwa ikiimarisha Maabara yake kwa kununua vifaa vya kisasa na kupanua wigo wa umahiri ikiwemo upimaji wa sumukuvu katika nafaka na mbegu.
Kwa lengo la kuhakikisha kuwa mgonjwa analindwa dhidi ya madhara yanayoweza kupatikana kwa kutumia dawa duni na bandia, TFDA imekuwa ikitekeleza mpango wa upimaji wa awali (preliminary screening) wa dawa za kifua kikuu, dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs), malaria pamoja na vijiua sumu (antibiotics) kwa kutumia Maabara Hamishika (Minilab kits) katika vituo vya forodha na baadhi ya hospitali za mikoa tangu mwaka 2002. Katika mpango huu, baadhi ya maabara hizi zinazohamishika 10, zitasambazwa katika vituo vya forodha vya Bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere pamoja na hospitali za mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Mtwara, Mara, Ruvuma, Tanga na Kigoma kwa ufadhili wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kama Management Sciences for Health (MSH) na katika kipindi cha 2007/2008 hadi 2012/2013, maabara hizi zimewezesha uchunguzi wa awali wastani wa sampuli 393 kwa mwaka.
Awamu ya pili ilihusisha usambazaji wa Maabara Hamishika tano (5) katika hospitali za mikoa ya Iringa, Rukwa, Manyara, Kagera na Kilimanjaro kwa ufadhili wa kampuni ya utengenezaji wa kemikali ijulikanayo kama Merck ya nchini Ujerumani, mwaka 2012. Ongezeko hili la vituo vitano (5) vya upimaji limewezesha wastani wa sampuli 1,485 kuchunguzwa kwa mwaka ukilinganisha na sampuli 393 kwa mwaka 2012/2013. Hili ni ongezeko la zaidi ya mara nne (4) ya idadi ya sampuli zilizokuwa zinapimwa kupitia maabara. Hali hii imewezesha idadi ya dawa duni kushuka kutoka 3.7% mwaka 2005 hadi kuwa chini ya 1% mwaka 2017. Kutokana na mafanikio haya, idadi ya dawa duni na bandia zinazobainika katika soko imeendelea kupungua kutoka wastani wa dawa tano (5) mwaka 2005 hadi dawa moja (1) mwaka 2017. Aidha, kupitia mpango huu, TFDA iliweza kubaini dawa bandia zilizodaiwa kuwa na viambata vya Ampicillin, Erythromycin, Quinine Sulphate, Metronidazole na dawa ya mseto ya Metakelfin.
Kutokana na mafanikio yaliyokwishapatikana kupitia mpango huu na kwa lengo la kuongeza idadi ya sampuli za kuchunguza, TFDA ilitenga fedha kiasi cha TZS 100 milioni katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya ununuzi wa Maabara Hamishika nyingine 10 na hivyo kufanya idadi ya maabara hizi kufikia 25 sasa kutoka 15 mwaka 2012/13. Ongezeko hili litaongeza idadi ya vituo vya uchunguzi na kuimarisha ufuatiliaji wa ubora wa dawa katika soko.
Maabara Hamishika zilizozinduliwa zinapelekwa katika ofisi tatu (3) za kanda za TFDA ambazo ni: Tabora (Magharibi), Mbeya (Nyanda za Juu Kusini) na Mtwara (Kusini). Aidha, nyingine zitapelekwa katika vituo vya forodha vya Namanga na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa KIA (Kanda ya Kaskazini), Sirari na Mtukula (Kanda ya Ziwa) na katika bandari ya Dar es Salaam (Kanda Mashariki). Vilevile Maabara nyingine itapelekwa katika hospitali za mikoa ya Geita na Katavi.
Pamoja na hatua hizi za kuongeza Minilab Kits kwa ajili ya uchunguzi wa awali ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara mpya ya TFDA Mwanza kwa ufadhili wa Mfuko wa “The Global Fund” unakamilika. Hatua hii inadhihirisha kuwa Mamlaka imejizatiti katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda afya ya jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa duni na bandia.
Udhibiti wa dawa duni na bandia (substandard and falsified medical products) bado ni changamoto katika nchi mbalimbali duniani na suala hili limekuwa agenda ya kudumu katika mikutano ya Mawaziri wa Afya duniani (World Health Assembly) kila mwaka. Suluhisho la kudumu ni kuendelea kuimarisha mamlaka za udhibiti kama inavyofanyika hapa Tanzania na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwani usambazaji wa dawa duni au bandia kutoka nchi moja kwenda nyingine hauhitaji visa. TFDA imejipanga vizuri katika EAC, SADC na pia ni mwakilishi wa nchi 47 za Afrika (WHO AFRO) katika Kamati Tendaji yenye wajumbe 12 duniani (member and Vice Chair of the Steering Committee of WHO Member State Mechanism on Substandar and Falsified Medical Products).
Aidha, Mamlaka itaendelea kuhakikisha kuwa maabara hii inaendelea kutambuliwa kitaifa na kimataifa kwa kukidhi vigezo vya ithibati ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na ISO/IEC 17025:2005 na hivyo kuendelea kushikilia vyeti vya umahiri tulivyo vipata mwaka 2011 na 2012.
Na. Joseph Lieme, Torinto Hot Blog. 17 hours ago
Maabara Hamishika zilizozinduliwa zinapelekwa katika ofisi tatu (3) za kanda za TFDA ambazo ni: Tabora (Magharibi), Mbeya (Nyanda za Juu Kusini) na Mtwara (Kusini). Aidha, nyingine zitapelekwa katika vituo vya forodha vya Namanga na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa KIA (Kanda ya Kaskazini), Sirari na Mtukula (Kanda ya Ziwa) na katika bandari ya Dar es Salaam (Kanda Mashariki). Vilevile Maabara nyingine itapelekwa katika hospitali za mikoa ya Geita na Katavi.
0 maoni:
Chapisha Maoni