Na HADIJA JUMANNE
Imepakiwa - Wednesday, January 25 2017 at 11:02
Kwa Mukhtasari
Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia taasisi ya kuendeleza elimu Afrika Mashariki (IED-EA) wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza wameanza utafiti wa kupima maendeleo ya shule za msingi katika ufundishaji nchini Tanzania.
DAR ES SALAAM, Tanzania
CHUO Kikuu cha Aga Khan kupitia taasisi ya kuendeleza elimu Afrika Mashariki (IED-EA) wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza wameanza utafiti wa kupima maendeleo ya shule za msingi katika ufundishaji nchini.
Utafiti huo pia utafanywa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Pretoria cha Afrika Kusini.
Akizindua mradi wa utafiti huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Elimu ya Juu kutoka wizara hiyo Profesa Sylivia Temu alisema utafiti huo ni wa miaka mitatu na utatekelezwa katika shule za msingi za Wilaya ya Temeke.
“Kinacholengwa zaidi ni kuwawezesha watoto kuwa na mchango katka mkakati mzima wa kujifunza, waweze kusema ni nini hawakijui na kitu gani wanakijua na wapi wana matatizo ili walimu wajue changamoto kwa ajili ya kufanyia kazi,” alisema Profesa Temu.
Alifafanua kuwa lengo la utafiti huo uliopewa jina la “Kupima kwa ajili ya kujifunza Afrika” (Afla) ni kusaidia wanafunzi kuelewa masomo yao.
“Utafiti huo ambao umelenga somo la Hisabati umeanza kutekelezwa katika shule zote za msingi zilizopo wilayani Temeke wakishirikiana na Chuo cha Ualimu Vikindu,” alisema Profesa Temu.
0 maoni:
Chapisha Maoni