Amesema makumbusho hayo ni kielelezo cha maisha na ustaarabu wa binadamu ambao unaelezea maisha ya vizazi vilivyopita.
“Makumbusho haya pia yatasaidia kujua sisi ni nani na tumetoka wapi,” amesema.
Amesema ujenzi wa makumbusho hayo utasaidia kuvutia watalii na wanasayansi wa masuala ya mambo kale duniani.
Samia amesema eneo la Ngorongoro lina historia kubwa ya maisha ya zamadamu ikibainika miaka 3 milioni iliyopita walikuwepo walioishi kwa kutembelea miguu miwili.
Amesema eneo la Ngorongoro kumebainika miaka 2.7 milioni iliyopita binadamu walianza kutumia zana za mawe katika kula nyama na kuwinda.
“Hapa ni chimbuko la historia ya zamadamu, Serikali itaendelea kulihifadhi na kulitunza eneo hili,” amesema.
Makamu wa Rais ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa kutoa fedha kugharimia ujenzi wa makumbusho hayo na miundombinu yake.
Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuwa na mkakati wa kutangaza makumbusho hayo ndani na nje ya nchi ili kuvutia zaidi watalii.
Pia, amewaomba wananchi wa Ngorongoro kuendelea kuhifadhi eneo hilo ikiwemo kutopeleka mifugo eneo la Creta. Amesema Serikali inajitahidi kuwaondolea kero zao likiwemo tatizo la maji.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema eneo la Ngorongoro ni la urithi wa dunia, hivyo wizara kwa kushirikiana na mamlaka wataendelea kulihifadhi na kulitunza.
Naibu Mhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, anayeshughulikia huduma za jamii, Asangye Bangu amesema ujenzi wa makumbusho hayo utasaidia kuongeza watalii.
Ametoa wito kwa mawakala wa utalii kuwapeleka watalii eneo la Olduvai Gorge ili kuongeza mapato kwa manufaa ya Taifa.
Meneja wa idara ya urithi wa tamaduni katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mhandisi Joseph Mwankunda amesema ujenzi wa eneo hilo umegharimu Sh1.7 bilioni.
Amesema makumbusho hayo ni ya kisasa zaidi duniani na wanatarajia yatadumu kwa zaidi ya miaka 50.
Meneja miradi katika Jumuiya ya Ulaya, Alexa Haden amesema jumuiya ya Ulaya imetoa fedha katika mradi huo kutokana na kuthamini mchango wa mambo ya kale.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha ameomba mafanikio ya mradi huo kugusa maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya mamlaka hiyo wanaokabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa maji.
0 maoni:
Chapisha Maoni