Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kutembelea eneo hilo kujionea changamoto za kimazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akiongea na Baraza la wafugaji (hawapo pichani) katika Wilaya ya Ngorongoro. Wafugaji hao walimweleza Waziri kilio cha muda mrefu cha mradi wa Josho Wilayani hapo, Waziri Makamba ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kuleta ufumbuzi mapema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kutembelea eneo hilo kujionea changamoto za kimazingira.
……………..
Na Lulu Mussa,Ngorongoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais mwenye dhamana ya usimamizi wa Mazingira nchini Mhe. January Makamba amesema kuwa ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti mimea inayohatarisha uoto wa asili katika Mamlaka ya Ngorongoro.
Katika kutatua changamoto hii, Waziri Makamba ameagiza kuundwa kwa jopo la wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Tecknolojia, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Hifadhi za Taifa za Tanzania, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Mamlaka ya Ngorongoro ndani ya miezi sita kufanyika kwa utafiti wa kina wa kisayansi wa kubaini mbinu mpya ya kupambana na mimea hiyo vamizi inayotawala mimea inayotumiwa na wanyama.
Akizungumza katika kikao kilichojumisha Wahifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro na Wajumbe wa Baraza la wafugaji, Waziri Makamba amesikitishwa na kitendo cha Uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro kushindwa kuandaa mpango kabambe wa usimamizi wa hifadhi baada ya ule wa awali kuisha muda wake. Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Ngorongoro kuandaa mpango huo mapema na kuwa shirikishi. ” Mpango mtakoandaa hakikisheni kuwa unakuwa shirikishi kwa jamii inayozunguka na wadau na Taasisi muhimu likiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri Makamba pia ameagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kimkakati wa Mazingira utakaojumuisha Wilaya nzima ya Ngorongoro na kuitaka Mamlaka ya Ngorongoro kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kutekeleza wajibu huo mapema. Ukaguzi huo wa kimkakati wa kimazingira kwa Wilaya hiyo unatazamiwa kutoa mtazamo wa hali ya mazingira kwa miaka hamsini ijayo.
Aidha, Waziri Makamba ameagiza kufanyika kwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira ama Ukaguzi wa Mazingira katika Hotel zote zilizopo eneo la hilo na kulitaka Baraza la Taifa la Hofadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupita siku ya Alhamisi tarehe 30/03/2016 kuwaandikia adhabu na kuwatoza faini wahusika wote ambao hawana vyeti hivyo. “Haiwezekani toka mwaka 2004 Sheria ipo na mpaka leo watu wanaendea na mchakato, hii haikubaliki!” Alisisitiza Makamba.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametoa miezi sita kwa wamiliki wa Hotel zilizopo katika Mamlaka ya Ngorongoro kuwekeza katika mfumo mpya wa kuvuta maji kutoka Mto Lukusale na kusitisha mfumo wa sasa wa kutoa maji kwenye creator. Pia Makamba ameutaka ungozi wa Mamlaka ya Ngorongoro ndani ya miezi sita kuandaa ramani itakayoonyesha mito na vijito vyote vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.
Waziri Makamba ametoa maagizo hayo leo juu ya namna bora ya kutumia rasilimali ya “creater” kwa ajili ya utalii na Uhifadhi wa Mazingira, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa zuio la mifugo ndani ya crater. Ziara maalumu na mahsusi ya kukagua utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira inayofanywa na Waziri Makamba hii leo imefika Wilayani Ngorongoro.
0 maoni:
Chapisha Maoni