Na Torintohot media Blog.
Na Mwandishi wetu Dar.
Kuhusu Mkutano huo amesema kufanyika kwake ni moja ya utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambapo Sura ya 4 ya Sera hiyo imeainisha lengo kuu ambalo ni kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa na kuondoa umasikini.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameeleza mafanikio ya sekta ya madini katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 ikiwemo kuongezeka kwa thamani ya madini yanayosafirishwa nje ya nchi kutoka Dola za Marekani bilioni 3.1 kwa mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 kwa mwaka 2022.
Mahimbali amebainisha hayo leo Oktoba 25, 2023 akizungimza katika Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2023 (TMIF) unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Mafanikio mengine amesema ni kuongezeka kwa ajira katika miradi mikubwa ya madini kutoka ajira 14,308 mwaka 2021 hadi ajira 16,462 mwaka 2022.
Kwamba kufuatia utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009, kiasi cha manunuzi ya bidhaa za ndani ya nchi katika miradi mikubwa ya madini kimeongezeka kutoka Dola za Marekani bilion 700 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani trilioni 1.1 mwaka 2022.
Amesema mafanikio hayo yamechochea sekta ya madini kukua kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 10.9 mwaka 2022.
“Sera ya Madini ya mwaka 2009 inalenga kuboresha mazingira ya usimamizi na udhibiti wa shughuli za madini ili kuvutia na kuendeleza uwekezaji wa Sekta binafsi katika Sekta ya Madini,” amesema Mahimbali.
Amesema ili kuhakikisha kuwa kunawekwa mazingira rafiki ya uwekezaji katika Sekta ya Madini, Mkutano huo hutumika kama jukwaa na hutoa fursa ya kupokea maoni kutoka kwa wadau wa Sekta ambayo hutumika kufanya maboresho ya Sera na Sheria za Madini ili kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.
Hivyo, katika Mkutano huu wa Mwaka 2023 yatafanyika majadiliano mbalimbali yatakayolenga kubaini fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.
Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi na wawakilishi wa Serikali za nchi mbalimbali duniani, viongozi wa dini, viongozi na wawakilishi wa Taasisi binafsi na Kampuni mbalimbali za uwekezaji za ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na Wataalamu na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.
Sambamba na hilo, mijadala hiyo inatarajiwa kutoa mapendekezo ya maeneo ya kuboresha Sera yetu ili iweke mazingira bora zaidi na rafiki ya uwekezaji.
0 maoni:
Chapisha Maoni