Torinto hot media Blog.
Jerome Mlaki wa DAR.
Mmiliki wa Kituo cha michezo cha Cambiasso, Kambi Zubeir, (kulia waliokaa), aliyekuwa kocha wa makipa wa klabu ya Simba, Muharami Mohamed (wa pili kulia) na wenzake wakiwa Kortini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam Jana baada ya kusomewa mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya kilo 34.
HATIMAYE aliyekuwa kocha wa makipa wa klabu ya Simba Muharami Sultan, mmiliki wa Kituo cha Michezo cha Cambiasso, Kambi Zubeir na wenzao wanne wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa Kilo 34.89.
Washtakiwa wengine ni Maulid Mzungu, Said Matwiko, Andrew John na Sarah Eliud walisomewa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliwasomea mashtaka, alidai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya.
Alidai katika shtaka la kwanza kuwa Oktoba 27, mwaka huu maeneo ya Kivule wilayani Ilala jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa Kilogramu 27.10.
Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Novemba 4, mwaka huu maeneo ya Kamegele Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa na dawa hizo zenye uzito wa Kilogramu 7.79.
Mwanga alidai kuwa upelelezi wa mashitaka hayo bado haujakamilika na kwamba aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mrio aliwataka washtakiwa hao kutojibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba makosa hayo hayana dhamana kisheria.
Hata hivyo Hakimu Mrio alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 5, mwaka huu na washtakiwa wapelekwe rumande.
0 maoni:
Chapisha Maoni