NA. Joseph Maiko, DAR ES SALAAM
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Herson Mwakyembe ameitaka Bodi ya ushauri ya Bodi ya Filamu Tanzania kuwasaidia wasanii wa filamu kwa kutoa ushauri wa kitaalamu hasa pale wanapotaka kuingia mikataba.
Akizungumza katika hafla ya Uzindua wa Bodi ya Ushauri ya bodi ya Filamu Tanzanja jijini Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe amesema kuwa mikataba mibovu ya wasanii wanayoingia imekuwa kikwazo katika kupiga hatua.
Amesema kuwa zipo changamoto nyingi katika tasnia ya Sanaa, hivyo anaamini kupitia bodi hiyo zitakwenda kupatiwa majibu katika kufanikisha Tanzania inakuwa na maendeleo.
"Naomba bodi ikafanye kazi ili kuwasaidia vijana wetu katika kuwashauri katika mambo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha haki za wasanii zinapatikana" amesema Dk. Mwakyembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Filamu Tanzania, Prof. Frowin Nyoni amesema kuwa mipango ya bodi ni kutoa ushauri katika kufanikisha mikakati mbalimbali ambayo imekusudiwa kufanyika.
Amesema kuwa baada ya miaka mitatu katika utendaji wao watakuwa wamefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo chanya kwa wasanii wa filamu.
Prof Nyoni ameeleza kuwa watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kwani wanatambua mchango wao katika kuleta maendeleo katika tasnia ya Filamu.
"Tutaangalia haki za wasanii ikiwemo mikataba mibovu, kupoteza kazi kwa kuibiwa pamoja na kutoa ushauri rafiki katika kufanikisha maendeleo ya sanaa hapa nchini" amesema Prof Nyoni.
Bodi ya ushauri ya bodi ya Filamu Tanzania inaongozwa na Prof Frowin Nyoni huku Katibu ni Yoyce Fissoo.
Wanachama wengine katika bodi hiyo ni pamoja na Dk. Vicensia Shule, Bishop Hiluka, Anuciata Leoapald, Kenneth Kasigila, Raymond Kwahelera pamoja na Jennifer Mgendi.
Katika hatua nyengine wadau mbalimbali wa tasnia ya Filamu nchini wamepewa tuzo mbalimbali za heshima kutokana na michango yao katika sanaa ya Filamu.
Miongoni mwa wadau walipokea tuzo za heshima ni pamoja na Shirikisho ka Filamu Tanzania, Ushirika la Utangazaji TBC, Azam Media pamoja na IPP Media.
0 maoni:
Chapisha Maoni