Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Aprili, 2018 umepungua hadi kufikia asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.9 ilivyokuwa mwezi Machi, 2018.
Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2018 imepungua ikilinganishwa na mwezi Machi, 2018.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Aprili, 2018 kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Aprili kumechangiwa na kushuka kwa gharama za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Aprili, 2018 zikilinganishwa na bei za mwezi Aprili, 2017”, alisema Bw. Kwesigabo.
Alitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na mahindi kupungua kwa asilimia 5.2, unga wa mahindi umepungua kwa asilimia 5.6, mtama kwa asilimia 7.3, unga wa muhogo kwa asilimia 9.3, maharage kwa asilimia 9.2 na mihogo mibichi kwa asilimia13.2.
Kwesigabo aliongeza kuwa mfumuko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya mfumuko wa bei wa mwezi Aprili, 2018 umepungua hadi asilimia 3.73 toka asilimia 4.18 mwezi Machi na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 1.8 toka asilimia 2.0 mwezi Machi, 2018
Mfumuko wa Bei ambao hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
0 maoni:
Chapisha Maoni