Na.
Jerome Mlaki.
Baada ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge
katika Pori la Akiba la Hifadhi ya Selous kutikisa Bunge, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewataka Watanzania
kutulia na kubainisha kuwa tathmini ya mradi huo inafanyika.
Makamba ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 23,
2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Redio
Clouds.
Jana bungeni mjini Dodoma mradi huo ulikuwa
gumzo wakati wabunge wakijadili bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya
mwaka wa fedha 2018/19, ambapo baadhi ya wawakilishi hao wa wananchi akiwemo
Nape Nnauye (Mtama) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), walitaka tathmini ifanyike
kabla ya kuanza kwa mradi huo.
Wamehoji kitendo cha Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) kutangaza tenda ya kukata miti katika pori hilo, tenda
inayohusisha ukataji miti zaidi ya mita za ujazo 3,495 na kwamba idadi ya miti
inayokatwa ni sawa na ukubwa wa Mkoa wa Dar es Salaam huku ikijulikana
wazi kuwa tathmini bado haijakamilika.
Katika maelezo yake ya leo, Makamba
amesema tathmini inafanyika ili kujua athari na namna ya
kukabiliana nazo, “lazima sheria ifuatwe ikiwamo kufanya tathmini ya athari ya
mazingira, ndicho kinachofanyika hivi sasa kuhusu mradi huo.”
“Tanesco walikuja NEMC (Baraza la Taifa la
Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira) kusajili mradi wa Stigle’s Gorge ili
kufanya tathmini ya mazingira. Baada ya kuandikisha Tanesco walimchagua mshauri
ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ni kazi ya kisayansi.”
Makamba amesema tayari shirika hilo
limeshapeleka ripoti katika ofisi yake baada ya kufanya tathmini hiyo na
kinachofuata ni NEMC kutuma timu kwa ajili ya kujiridhisha kuhusu
yaliyoandikwa katika mradi na yanayoonekana kama ni kweli.
Amesema baada ya hapo kamati ya ufundi ya
ushauri itazungumza na wadau wote katika eneo la mradi na kuthibitisha
taarifa zilizopo kuhusu mradi husika.
0 maoni:
Chapisha Maoni