Na Jerome Mlaki wa Dar. 0789106710


DAR ES SALAAM — 

Kampuni ya Zara Tanzania Adventures imeendelea kuunga mkono juhudi za kukuza utalii wa ndani nchini kwa kuwaunganisha Watanzania na vivutio mbalimbali vya utalii, kupitia kampeni ya ‘Twenzetu Kileleni’ inayolenga kuwahamasisha wananchi kutembelea na kujionea utajiri wa rasilimali za taifa.

Kampeni hiyo imeingia msimu wake wa tano na inalenga kuwapeleka mamia ya Watanzania kileleni mwa Mlima Kilimanjaro, huku pia ikitoa fursa kwa wananchi ambao hawawezi kupanda mlima huo kutembelea vivutio vingine kwa gharama nafuu.

Kampeni hiyo imezinduliwa Septemba 10, 2026, katika Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika yenye kaulimbiu inayosisitiza umoja wa Taifa na kilele cha Afrika.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Zara Tanzania Adventures, Zainab Ansell, amesema zaidi ya washiriki 200 wanatarajiwa kushiriki katika safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Marangu, huku ushiriki wa vijana ukitarajiwa kuongeza idadi hiyo hadi zaidi ya watu 400.

Amesema safari hiyo haitalenga kupanda mlima pekee, bali pia itaunganisha utalii na uhifadhi wa mazingira, ambapo washiriki watashiriki shughuli za upandaji miti kabla ya kuanza safari.

Ansell amesema kwa Watanzania ambao hawataweza kupanda Kilimanjaro, kampeni hiyo imeandaa fursa za kutembelea hifadhi na vivutio vya Serengeti, Ziwa Manyara na Ngorongoro kwa gharama nafuu.

Amesema Watanzania wanapaswa kutumia kipindi cha Desemba kutembelea vivutio hivyo, akibainisha kuwa wageni kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakifika nchini kwa ajili ya kupanda Kilimanjaro, hivyo wananchi wa ndani wanapaswa pia kutumia fursa hiyo kujionea utajiri wa rasilimali walizonazo.

Kwa upande wake, Faustin John kutoka Zara Tanzania Adventures amesema maandalizi yamekamilika kuhakikisha washiriki wanapata huduma zote muhimu, zikiwemo malazi, chakula, mavazi, waongoza watalii pamoja na elimu ya mazingira.

Amesema njia ya Marangu imepewa kipaumbele kutokana na uwepo wa huduma za malazi na mazingira yake kuwa rafiki kwa msimu wa mvua, huku safari ya kufika kileleni ikitarajiwa kuchukua siku sita.

Ofisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Albert Mboto, amesema kampeni hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali za kukuza utalii wa ndani na kuwahamasisha Watanzania kutumia vivutio vilivyopo nchini.

Naye Mary Maduhu kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii amesema wanafunzi na watumishi wa chuo hicho watanufaika na kampeni hiyo kwa kupata uzoefu wa vitendo katika utalii wa milimani, uhifadhi na usimamizi wa urithi wa taifa.

Kwa upande wake, mwakilishi wa TTCL, Peter Mwambuga, amesema kampuni hiyo imeboresha huduma za mawasiliano kuanzia eneo la geti la Marangu hadi kileleni mwa Mlima Kilimanjaro.

Akizungumza kuhusu ushiriki wa Watanzania katika kampeni hiyo, John ametoa wito kwa viongozi wa Serikali, wabunge, mawaziri, taasisi binafsi, viongozi wa dini, mabalozi na wananchi kwa ujumla wanakaribishwa kushiriki.