WELCOME TORINTO HOT MEDIA BLOG | FOR MORE INFORMATION ABOUT OUR NEWS CONTACT US CELL: +255 756 188 180 | Email: josephlieme@gmail.com| KARIBU TORINTO HOT MEDIA BLOG | KWA MAELEZO ZAIDI KUHUSU HABARI ZETU WASILIANA NASI SIMU: +255 756 188 180 | Barua Pepe: josephlieme@gmail.com | DO YOU NEED TO DEVELOP YOUR BLOG CONTACT US CLICK HERE | JE UNAHITAJI KUBORESHA BLOG YAKO WASILIANA NASI BOFYA HAPA

Jumanne, 29 Septemba 2026

 21:17      No comments


Na Jerome Mlaki wa Dar.

Serikali imesema kuwa,itaendelea kuwajali watu wenye ulemavu ikiwemo kutekeleza mpango wa Taifa wa watu wenye ualbino.

Akizungumza , Septemba 28, 2026, wakati akifungua Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa MTHUWWU jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema hatua hizo zinapaswa kuambatana na utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yote yanayohusu haki na ustawi wa watu wenye ualbino.

Kabudi amesema Serikali na wadau wana wajibu kuhakikisha mpango huo hautabaki kwenye nyaraka, bali utekelezwe kwa vitendo, ukipewa rasilimali na kutekelezwa kwa wakati.

“Ni muhimu kuweka mipango madhubuti ya utekelezaji wa mpango na kuhakikisha kuwa mikakati na afua zilizoainishwa katika mpango zinapatiwa rasilimali na kutekelezwa kwa wakati,” amesema.

Amesema shughuli zilizopangwa zinapaswa kutekelezwa na taarifa zake kutolewa kwa wakati ili kuwezesha Serikali na wadau kufuatilia maendeleo, kubaini changamoto, kupima matokeo na kuchukua hatua za kuboresha utekelezaji.

Kabudi amesema mpango huo una nguzo nne ambazo ni ulinzi, kinga, usawa na kutobagua pamoja na uwajibikaji, huku mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ukitakiwa kufanya kazi kuanzia ngazi ya Taifa hadi Mkoa, Halmashauri, kata, kijiji na mtaa.

Akizungumza katika mkutano huo afisa ustawi wa jamii mkuu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Joy Maongezi amesema imetenga Sh milioni 90 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga dhidi ya saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino, huku ikiagiza wadau wote kuhakikisha Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu wenye Ualbino (MTHUWWU) unatekelezwa kwa vitendo na kwa wakati.

 Amesema fedha hizo zimetengwa katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

Amesema tayari chupa 339 za mafuta hayo zimesambazwa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau.

Maongezi amesema Serikali pia ina wataalamu takribani 403 wa ngozi katika halmashauri pamoja na madaktari bingwa wa ngozi 98 katika hospitali za kanda na rufaa za mikoa.

Amesema jukwaa hilo la siku tatu linapaswa kwenda zaidi ya kutathmini yaliyofanyika, bali kubaini mambo yanayotakiwa kutekelezwa, maeneo yenye upungufu na hatua mahsusi za kuziba mapengo hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wambura Kizito, amesema sasa ni wakati wa kutoka katika hatua ya kuwa na mpango kazi na kuingia kwenye utekelezaji unaopimika, unaoratibiwa na wenye uwajibikaji.

Amesema masuala ya watu wenye ualbino ni mtambuka na hayawezi kutekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu au taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa sekta za afya, elimu, ajira, haki na ulinzi, ustawi wa jamii, uwezeshaji wa kiuchumi, ulinzi wa mtoto na usalama.

Amesema jukwaa hilo litabaini shughuli zilizotekelezwa, zinazoendelea na ambazo hazijatekelezwa pamoja na sababu zake, taasisi zinazohusika, rasilimali zinazohitajika na changamoto zinazokwamisha utekelezaji.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Uratibu na Utekelezaji wa MTHUWWU, Yohana Sali, amesema jukwaa hilo litatoa nafasi kwa Serikali na wadau kujadili mafanikio, changamoto, fursa na vipaumbele vya utekelezaji wa mpango huo.

Amesema siku ya kwanza itajikita katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mpango huo, historia yake, maudhui na hali ya utekelezaji, huku siku ya tatu ikijikita katika uratibu, masuala mtambuka na maandalizi ya mpango wa utekelezaji.

Kabudi amesema Serikali pia inaendelea kuboresha mifumo ya taarifa za watu wenye ulemavu hadi ngazi ya kijiji na mtaa.

Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania Bara ina watu wenye ualbino 71,631, wakiwemo wanaume 41,203 na wanawake 30,428.

Amesema taarifa hizo zinaisaidia Serikali kufahamu idadi na maeneo wanakoishi watu wenye ualbino ili kupanga huduma kwa kuzingatia mazingira na mahitaji yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kutokomeza mauaji na ukatili dhidi yao, huku akibainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo mpya unatoa matumaini makubwa katika kuboresha maisha yao na fursa sawa za elimu, ajira na huduma za afya.

Hata hivyo Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Kurasa

Translate

Popular Posts

Blog Archive

Tangazo!

JE UNAHITAJI KUBORESHA BLOG YAKO?

WEIGHT MANAGEMENT

WEIGHT MANAGEMENT

SIKILIZA NYIMBO MPYA

Watembeleaji

On Facebook

Tangazo Victoria!!

Date & Time

Weight Management



CLICK THIS IMAGE

Sikiliza Clouds Radio



Sikiliza Kwanza Jamii Radio

Total Pageviews

Fomu ya Anwani

Jina

Barua pepe *

Ujumbe *