Jumatano, Novemba 13, 2023
Digital online
Torintohot media Blog.
Na. Jerome Mlaki wa Dar
- Imeelezwa kuwa taarifa zinazotolewa na wananchi ndizo zinaiwezesha Serikali kubadilisha hali zao za maisha kwa kuwaletea maendeleo.
- Unguja. Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Salum Kassim Ali amesema taarifa zinazotolewa na wananchi ndizo zinazoiwezesha Serikali kubadilisha hali zao za maisha kwa kuwaletea maendelo.Akizungumza hayo leo, Novemba 13, katika kikao cha usambazaji na matumizi ya matokeo ya viashiria vya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Polisi Ziwani, ameeleza kuwa kuna kila sababu ya wananchi kupatiwa uwelewa wa umuhimu wa kutoa taarifa sahihi ili kuweka mipango madhubuti katika upatikanaji wa huduma.
"Matokeo ya Sensa ni muhimu kwani yanasaidia kupanga, kusimamia na kubadilisha maisha ya wananchi na kuwaweka katika hali nzuri," amesema Salum.
Mtakwimu huyo, alibainisha kuwa takwimu ya idadi ya watu na makazi itasaidia kusimamia mchakato wa kutoa huduma ikiwemo huduma za afya kwa wananchi kwani lengo ni kuongeza ufanisi wa maendeleo nchini.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibu, Idrissa Kitwana Mustafa amesema iwapo matokeo hayo yatatumika vizuri basi ni wazi kuwa jamii itaweza kupanga mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Amesema kuwa takwimu hizo zitasaidia kuweka rasilimali ambazo zinatumika kukuza uchumi wa taifa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa jamii.
"Takwimu hizi zitasaidia kupatikana huduma za jamii kwa urahisi hivyo nawataka viongozi kutumia matokeo hayo katika ugawaji wa rasilimali kwa kuongeza maendeleo nchini," amesema Kitwana.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa masheha na madiwani kuwa mstari wa mbele katika kufikisha taarifa hizo kwa jamii ili kuisaidia serikali kutoa huduma sahihi kwa wananchi.
Pia, Kitwana amewataka watendaji wa ngazi za Wadi na Shehia kuyatumia matokeo ya Sensa kuleta mabadiliko kwenye maeneo yao.
Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Hamza Haji amesema kwa mujibu wa matokeo ya Sensa 2022, imeonesha kuwa Mkoa wa Mjini Magharibi una idadi kubwa ya wakazi ikilinganishwa na mikoa mingine ya Zanzibar.Hata hivyo ametoa pongezi kwa masheha kufanikisha kazi hiyo kuanzia ngazi ya matayarisho hadi upatikanaji wa matokeo mazuri.
0 maoni:
Chapisha Maoni