Mama mmoja afahamika kwa jina la Editha Wambura, amejikuta akilala nje jana mara baada ya taasisi inayojishughulisha na udalali hapa nchini, YONO kuifunga nyumba yake yenye namba 58, iliyoko Kata ya Mikocheni mtaa wa Mpungani, na kumtoa nje yeye pamoja na mtoto huku wakidai agizo hilo limetoka RITA .
Tukio hilo la kutolewa mama huyo nje ya lilitokea jana jioni huku chanzo cha kufungwa kwa nyumba hiyo kikidaiwa ni zuio kutoka kwa ndugu wa marehemu ambao wanashirikiana na RITA ambao ndio wasimamizi wa Mirathi huku wakiamuru YONO kufungia Nyumba hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari kwenye eneo la Nyumba hiyo, Editha Wambura, ambaye ni mke wa Marehemu ,James Wambura, amesema chanzo cha mgogoro huo ilitokea mara baada ya mumewe kufariki na kuacha baadhi ya mali ambazo ndugu zake walijitokeza na kuzidai.
Amesema kuwa, baada ya kufariki mumewe mwaka 2012, kuliibuka mizozo mbali mbali huku ndugu wa mume wakimletea baadhi ya wanawake wakidai amezaa nao watoto 11.
Aidha, amesema kabla ya mumewe kufariki hajawahi kuwaona hao watoto lakini leo analetewa, miongoni mwa wakina mama waliowaleta watoto hao ni pamoja na wafanyakazi wa Bar na mwalimu ambaye alimfundisha mtoto wake alivyokuwa chekechea.
"Nashangaa sana ndugu waandishi, mimi na mume wangu tumefunga ndoa 1995, mpaka sasa tumebahatika kupata watoto 3, mmoja yupo darasa la saba na wengine wapo chuo mwaka wa kwanza, kwani nini leo wanaletwa hawa, kuna namna hapa inafanyika kunidhurumu mali zangu nahangaika sana na hawa watoto nalipia ada, kula na maradhi juu yangu je wakichukua na hii mali iliyobakia tutaishi vipi?"aliuliza mama huyo akionekana na uchungu mkubwa sana.
Ameongeza kuwa, mpaka sasa wana miaka 18 katika nyumba hiyo wanaishi hapo, amekuwa mtu wa kufuatiliwa sana na Yono pamoja na Rita, amesema Rita ndio wasimamizi wa Mirathi lakini hawatendi haki wanaangalia upande wa ndugu wa marehemu, Mahakama haijatoa idhini yoyote ya kuondoka kwenye nyumba hiyo, kwanini wao wamechukua majukumu ya kumtoa nje? hii ni mara ya pili kuchukua vitu vyake vya ndani na kununua upya, hivyo amesema kuwa watu hao wanafanya unyanyasaji kwani hawafuati sheria wamekuwa watu wa kutumia nguvu pasipo na haki kutendeka.
Pia ametaja baadhi ya mali ambazo amechukuliwa, miongoni mwa mali hizo ni pamoja na fedha, magari 2, vifaa vya Ofisi, Msasani klabu, Trekta 2.
Mama huyo amesema kuwa, alitegemea RITA wangekuwa msaada kwake lakini cha kushangaza wao ndo wanamnyanyasa wakati kesi hiyo bado ipo Mahakama Kuu na haijatolewa ufumbuzi.
Ameiomba Serikali ya Rais Magufuli, Waziri husika wa Sheria na Waziri wa Ardhi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na Mkuu wa Wilaya kuingilia kati suala hilo ili kuhakikisha kwamba anapata haki zake zote ikiwemo zile walizochukua mwanzo.
Kwa Upande wake kaimu Meneja wa masuala ya ufilisi na udhamini, RITA, Reinald Makoko, amesema kuwa kuhusiana na suala zima la usimamizi wa mirathi ya Marehemu James Wambura, ni kwamba waliteuliwa na Mahakama kuu tarehe 23/5/2014 kusimamia mirathi hiyo mara baada ya mgogoro baina ya warithi kutokuafikiana,hivyo Mahakama ikaona kwamba kabiziwasi mkuu ndiye mtu pekee ambaye anawea kusimamia mirathi hiyo.
Hivyo baada ya kufuata sheria jana wakafanikiwa kumuondoa mama huyo kwenye hiyo nyumba kuhakikisha inauzwa au kupangishwa ili warithi wote waweze kupata stahili yao.
"Mamama huyo sio mrithi, ni mtalaka wa muda mrefu wa Marehemu, lakini ana haki ya kufuatilia sehemu ya mirathi hiyo ambayo ni stahili ya watoto wake watatu aliozaa na Marehemu, hivyo ilikuwa ni sahihi kumuondoa kwenye nyumba hiyo ili haki itendeke kwa warithi wote ikiwemo watoto alionao yeye"amesema Mkoko
Aidha ametoa wito na kusema kuwa upo umuhimu wa kuandika wosia kwa sababu itasaidia sana kuepusha migogoro ambayo inawez kutokea baada ya mtu kufariki, hususani ni pale panapokuwa na warithi wengi au warithi mbali mbali wanaotoka kwenye matumbo tofauti, kwa mfano baba amezaa na wanawake wawili wale watoto kukaa pamoja na kuelewana ni vigumu , hivyo tunawakaribisha wananchi kuja kwa ajili ya kuandika wosia kwa sababu Ofisi hiyo inaandika wosia kwa manufaa ambayo warithi watapenda mtu anufaike baada ya marehemu kufariki dunia.
0 maoni:
Chapisha Maoni