Na Joe Clanx
WANANCHI katika kijiji cha Maore wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, wamesema tatizo la vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga vinachangiwa na upungufu wa watumishi katika zahanati ya kijiji pamoja na ufinyu wa wodi ya wazazi iliyopo.
Wakitoa maoni yao katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Taasisi ya Utepe mweupe (White Ribbon) kujadili vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga katika kijiji cha Maore wilayani Same wananchi hao wameiomba serikali kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo.
Mbali na changamoto hizo wakazi wa Maore wameeleza pia changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi wa kike kupata ujauzito pindi wawapo shuleni kuna changiwa na wazazi kushindwa kuwaeleza ukweli watoto wao kuhusu kuanza mahusiano wawapo shuleni.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Same, Dk. Godfrey Andrew amesema vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga vimepungua wilayani Same hadi kufikia 15 mwaka huu ukilinganisha na vifo 60 vilivyotokea katika miaka miwili iliyopita ya 2015 na 2016 huku akibainisha mikakati iliyopo ya kupambana na changamoto za upungufu wa watumishi.
Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe kitaifa (The White Ribbon Alliance) Rose Mlay amesema kuwekeza kwa mama mjauzito kunachangia kuzaliwa kwa kijana mwenye afya njema atakayechangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kulea maendeleo.
Same ni mojawapo ya wilaya saba zilizoko katika Mkoa wa Kilimanjaro zinazokabiliwa na changamoto ya vifo vya akina mama wajawazito vitokanavyo na uzazi huku sababu ya vifo hivyo kwa kina mama ikielezwa kuwa ni Kifafa cha Mimba, kupasuka kwa mji wa mimba na kutokwa na damu nyingi.
0 maoni:
Chapisha Maoni